BEN POL AELEZA SABABU ZILIZOPELEKEA AVRIL KUTOONEKANA KWENYE VIDEO YA ‘NINGEFANYAJE’

Dar
es Salaam, Tanzania
– December 28, 2015  – Siku chache baada ya kuachia video ya wimbo
wake – ‘NINGEFANYAJE’, muimbaji wa
R&B kutoka Tanzania, Bernard Paul 
maarufu kama Ben Pol ameeleza
sababu zilizopelekea muimbaji  Avril kutoka Kenya aliyeshirikishwa
kwenye wimbo huo,  kutoonekana kwenye video
hiyo anayoitaja kuwa kubwa kuliko video zote alizowahi kufanya.
Katika video hiyo iliyoongozwa na Justin Campos wa Afrika
Kusini, Ben Pol anaonekana akiimba
na Rossie M  ambaye pia ameshirikishwa
kwenye wimbo huo huku mashabiki wakiisikia sauti ya Avril bila kumuona mwimbaji huyo mrembo.
Ben
Pol

amewaomba radhi mashabiki wake kwa kuwapa video ambayo haijakamilisha wahusika
wote hususan kutokuonekana kwa Avril,  na kwamba sababu zilizopelekea hivyo zilikuwa
nje ya uwezo wa pande zote katika utayarishaji wa video hiyo.

Ben
amesema kuwa baada ya yeye na Rossie M kuwasili Afrika Kusini ilikoshutiwa
video hiyo, zilijitokeza changamoto muda mfupi kabla ya kuanza zoezi hilo. Ben Pol ameeleza kuwa pamoja na kuwa na
maandalizi makubwa, video ya ‘Ningefanyaje’
ilikumbwa na changamoto nyingi tangu awali zilizopelekea kuahirishwa mara tatu.  

“Kwa kweli hii video tokea mwanzo ilikuwa na
changamoto, kwanza tuliisogeza mbele karibu mara tatu tena tukiwa tayari
tumeshafika Afrika Kusini mimi na Rossie,” alisema Ben Pol. “Mara ya kwanza ni kutokana na ‘delay’ ya viza upande wa Avril. Si unajua Wakenya wao wanaenda
South kwa viza tofauti na sisi Tanzania hatuendi kwa viza so kwetu ni rahisi
zaidi muda wowote tu ukiamua fasta unaenda,” aliongeza.
Mkali huyo alieleza kuwa baada ya terehe mpya
kupangwa na muongozaji aliyeshuti video hiyo, Justin Campos, siku moja kabla ya
kushuti, AVRIL alipata tatizo lingine ambalo lilimzuia kusafiri kwa siku
iliyofata kwenda Afrika Kusini. 
Wakati huo huo, Campos naye alimueleza Ben Pol kuwa  kwa jinsi ratiba yake ilivyo endapo
ataahirisha tena kushuti video hiyo, ratiba yake isingemruhusu kushuti video
hiyo hadi Januari au Februari 2016,  kitu
ambacho Ben Pol amesema  kisingewezekana kwasababu ingeendelea
kumgharimu zaidi kifedha na kuvuruga ‘timing’ yake.
“Kutokana na hali hiyo, sikuwa na jinsi nyingine
zaidi ya kukubali matokeo kwasababu 
mwisho wa siku si mimi wala Avril
wala director aliyekwamisha bali ni ‘situation’ ambayo ilikuwa nje ya uwezo wa
kibinadamu.” Ben Pol anaeleza.
Ameongezea kuwa pamoja na kwamba angeweza kuamua
kushuti video kwa kutumia version nyingine ya wimbo huo isiyokuwa na sauti ya Avril ili video isionekane na upungufu
wake, lakini hakupenda kufanya hivyo kwa kuwa lengo kuu la wimbo lilikuwa
kumshirikisha mwimbaji huyo. Pia, mashabiki wangekosa ladha nzuri na kazi nzuri
aliyoifanya Avril.  Hivyo, aliamua kufanya video hiyo bila Avril na kukusudia kuwaeleza mashabiki
wake kilichosababisha hali hiyo kwa kuwa aliamini mashabiki wataelewa magumu
aliyopitia katika kuwapa video hiyo waliyokuwa wakiisubiri.
“Namshukuru sana Avril kwa kukubali kufanya kazi na mimi kwasababu imetimiza moja
kati ya malengo yangu ya 2015, ambayo ilikuwa kuanza kufanya kazi na wasanii wa
nje ya Tanzania na yeye ndiye alikuwa chaguo langu la kwanza. Ni imani yangu tutafanya
tena project nyingine ya pamoja na kuikamilisha kama tulivyoikusudia,” alimaliza
Ben Pol na kuwashukuru  mashabiki wake kwa kuupokea kwa mtazamo
chanya wimbo na video yake.

Tazama  NINGEFANYAJE’  YouTube: https://youtu.be/iuUdNwR06BE
JIUNGE NAMI KUPITIA 
Twitter: @djmwanga     
Instagram: @djmwanga     
Facebook Fans Page: DJMwanga

ad

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *