Black Coffee Ni Nani Na Kwanini Ameshinda Tuzo Za BET? @RealBlackCoffee

Jina la Black Coffee,
Sio jina linalotambulika sana miongoni mwa watanzania. Mimi binafsi
nilianza kufuatilia kazi zake baada ya kutajwa kuwa miongoni mwa
wanamuziki wanaowania tuzo za BET za mwaka huu katika kipengele cha Best
International Act-Africa akiwemo Diamond Platinumz. Nikiri kwamba
sikumfahamu mpaka mapema mwaka huu.
Haishangazi kuona kwamba baada ya kushinda tuzo ya BET katika kipengele
cha Best International Act-Africa hapo jana, watanzania wengi
hatukuamini. Wengine walighafilika kabisa na kufanya kitendo ambacho
naweza kukiita sio cha kiungwana. Baadhi waliingia kwenye kurasa za
Instagram za Black Coffee na BET Africa na kubwaga mioyo yao.
Walioingia kwenye ukurasa wa BET Africa na
kuelezea hisia zao,siwezi kuwalaumu sana. Unaposhindana unategemea
kushinda.Ukishindwa habari ya asiyekubali kushindwa sio mshindani,huweza
kuyeyuka. Cha ajabu ni tulipoamua kumwagia upupu wa kejeli na matusi Black Coffee kwenye kurasa zake binafsi. Yeye katangazwa mshindi. Akatae? Kosa lake lipo wapi? Kahonga ili ashinde?
Kitendo kile sio cha kiungwana hata kidogo. Tulitakiwa kuelezea hisia
zetu kwa staha,ustaarabu na uungwana. Vinginevyo tunahatarisha
kuwaharibia wasanii wetu hata teuzi za mbeleni. Na wala sio jambo baya
kumpongeza mshindi. Ndio ushindani wa kweli. Unapokwenda kushindana,
kuna kushinda na kushindwa. Tumeshawahi kushinda. Hatukumiminiwa matusi.
Kwanini kwetu iwe tofauti?
Lakini Black Coffee ni nani? Iweje ashinde tuzo za BET ilhali wewe
humfahamu au hujawahi kusikia kazi zake kabla ya jana? Kwa mujibu wa
vyanzo mbalimbali vya mtandaoni ikiweko Wikipedia na vyombo vya habari
vya Afrika Kusini na kwingineko duniani, jina lake kamili ni Nkosinathi Innocent Maphumulo na alizaliwa tarehe 11 March 1976 huko eThekwini, Durban.
Black Coffee BET Awards Best International Act 2016-Winner
Alianza kujishughulisha rasmi na muziki mwaka 1995 kama DJ na Producer.
Mpaka sasa ana albums 5. Kama unapenda kazi za David Guetta wa Ufaransa
unaweza kufananisha anachokifanya Black Coffee na DJ huyo na wengine
duniani kama DJ Khaled nk.
Inaaminika kwamba kwa upande wa Africa, Black Coffee ni miongoni mwa DJs
na Producers mabingwa. Huko Afrika Kusini ameshashinda tuzo kadhaa
ikiwemo ya mwaka 2015 ya Breakthrough DJ Of The Year katika tuzo za DJs
(DJ Awards) zilizofanyikia Ibiza, Spain. Tuzo hiyo ilifuatia kutoa album
yake ya 5 ya Pieces Of Me. Black Coffee pia anamiliki record label
Soulistic Music. Ameshashinda tuzo nyingine kadhaa zikiwemo za South
Africa Music Awards(SAMA) na Chanel O.
Kwa hiyo ukiangalia kutokea alipoanza mwaka 1995 mpaka hapa alipofikia
hivi sasa ni kwamba amepitia mengi ikiwemo kushindanishwa, kushinda na
kushindwa. Historia yake inasema kuteuliwa kwake kushiriki katika Red
Bull Music Academy mwaka 2004 huko Cape Town ndiko kulimuweka kwenye
ramani ya dunia. Red Bull Music Academyni jukwaa la kimataifa la
kuvumbua vipaji. Naamini pale ndipo alipojiweka “kimataifa”. Ni njia
muhimu.
Kama wanamuziki wengine wanavyofanya, ili ujulikane kimataifa unaweza
pia kushirikiana na wasanii wengine wakubwa duniani. Kwa bahati nzuri au
mbaya, yeye hakuhitaji kwenda mbali sana nje ya Afrika Kusini ambapo
kuna majina kama Hugh Masekela, Busi Mhlongo,DJ Shimza, Yvonne
ChakaChaka nk.
Katika kushirikiana na majina hayo makubwa, mwaka 2005 Black Coffee
aliufanyia DJ sampling wimbo maarufu wa Hugh Masekela uitwao Stimela
(1972). Hugh Masekelani
legend wa Afrika. Alimshirikisha katika album yake ya kwanza aliyoipa
jina lake Black Coffee. Unaweza kuona jinsi gani wimbo huo ulimsaidia
Black Coffee.
Kabla ya hapo alienda shule kusomea muziki wa Jazz katika chuo cha
muziki chaTechnikon Natal. Na kabla ya hapo alikuwa miongoni mwa
waimbaji wasaidizi wa Madala Kunene pamoja na wanafunzi wenzake
wanafunzi wenzake, Mngobi Mdabe(Shota) na Thandukwazi
Sikhosana(Demor).Madala Kunene ni miongoni mwa wanamuziki wa Afrika
wanaosifika kwa kupiga muziki wa Afrika asilia. Vibao vya Kunene kama
vile UbomboMlisaAbangoma nk vinaweza kukupa picha ya alipotoka Black Coffee.
Baadae akishirikiana na Mngobi Mdabe(Shota) na Thandukwazi
Sikhosana(Demor) waliunda kundi la muziki wa Afro-Pop walilolipa jina
SHANA ikiwa ni kifupi cha Simply Hot and Naturally African. Baadae aliamua kwenda kivyake.
Kingine ambacho naamini kimemfikisha Black Coffee hapa alipofika ni
“branding”.Ukimfuatilia kwenye tovuti yake rasmi, kwa mfano, utaona
kwamba amejiweka kibiashara haswa..Ni kama vile anajiandaa kufika mahali
fulani. Huwezi kuwa msanii hivi leo halafu ukawa huna tovuti
inayoeleweka.Inaonekana wazi kabisa kwamba nyuma yake wapo watu makini
sana wanaosimamia kazi zake au kushirikiana naye.
Kingine ambacho bila shaka BET Awards Academy wamekiona ni jinsi ambavyo
Black Coffee katika nyimbo zake anajaribu sana kuhifadhi ile ladha ya
muziki wa kiafrika au tuseme wa Afrika Kusini. Originality ni miongoni
mwa vitu vinavyozingatiwa na kuheshimiwa sana katika utoaji wa tuzo.
Red Bull Taster ZA 09
Kwa hiyo unaweza kuona kwamba kushinda kwake tuzo ya BET sio ajali kubwa
kuliko zingine zozote kuwahi kutokea. Hatujashindwa na bwege. Lipo la
kujifunza. Na kwa namna moja au nyingine (ingawa hata mimi nilitamani
Diamond Platinumz ashinde) hakushinda kwa ngekewa tu.
Kinachotia moyo ni kwamba mwanetu Diamond Platinumz haonyeshi kubeza
hata kidogo kazi za Black Coffee. Kupitia ukurasa wake wa Instagram
amempongeza na kumtakia kila la kheri. Huo ndio uungwana na moyo wa
ushindani. Anajua kuna mwakani na kuna tuzo zingine. Ushindi upo tu.
Isitoshe kama video zetu karibu zote tunafanyia South Afrika siku hizi,
uadui hauwezi kutusaidia.
Black Coffee na mkewe Mbali Mlotshwa
Mwaka 2011 Black Coffee alimuoa mwigizaji na mtangazaji wa televisheni,
Mbali Mlotshwa. Wana watoto wanne Esona, Lilitha, Anesu na Asante.
Wawili kati ya hao ni kutoka kwenye mahusiano yake kabla ya kumuoa
Mbali.
Ratiba yake inaonyesha kwamba kuanzia mwezi ujao wa Julai mpaka October
ana tour katika nchi za Marekani, Spain, Switzerland, Germany,
Greece,Belgium na Afrika Kusini. Mwaka huu tayari ameshiriki katika
matamasha makubwa ya muziki dunianiCoachella Valley Music and Arts
Festival na Ultra Music Festival.
Hatujashindwa na bwege. Tunalo la kujifunza.
cc: Jeff Msangi

Download DJMwanga Android Application Click HERE

https://goo.gl/Dpx8j4
JIUNGE NAMI KUPITIA 
Twitter: @djmwanga     
Instagram: @djmwanga     
Facebook Fans Page: DJMwanga
ad

7 thoughts on “Black Coffee Ni Nani Na Kwanini Ameshinda Tuzo Za BET? @RealBlackCoffee

  1. Historia sio shida bro, tatizo ni kwamba kwa mwaka jana amefanya nn cha ajabu mpaka ashinde? Ngoma zilizovuma Afrika nzima hakuna ngoma ya huyo jamaa, wapo akina wana Nigeria kibao ambao walitamba mwaka jana akiwemo platnumz lakini Black coffee hakufanya lolote, umejaribu kuongelea historia yake lakini hujatoa sababu kwa nn ashinde tuzo, mimi binafsi naona hiyo tuzo kupewa tu, coz kwa Afrika wasanii waliotisha mwakajana na kua the best wanafahamika, ila black coffee hayumo.

  2. Sisi wabongo ni wagumu kuelewa kama Diamond platnumz amekubali kushindwa katika pambano wewe shabiki unataka ufanye nini sasa..?
    Wengi wetu tumemzoe davido,wizkid,mafikizoro n.k,lakin bado wapo wengi ambao hatuwafaham mi naona amestahili kuvuna alichokipanda ila mwanetu Diamond aongeze spead na kupeperusha bendera ya Tanzania….

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *